07 May 2012

                                     KWA NINI HUJIAMINI MPENDWA?

KUJIAMINI NI MUHIMU
Hili ni tatizo la kisaikolojia zaidi kwa sababu kuna baadhi ya watu wanakosa kujiamini. Kuna mwingine anaweza akakaa kwenye kioo kwa saa kadhaa na kuanza kujitoa kasoro katika mwili wake.
Hujiona mbaya asiyevutia na ambaye hana thamani kabisa katika ulimwengu wa mapenzi, hujiona hawezi kupata mpenzi katika maisha yake yote baada ya kujitoa kasoro hizo. Mwingine hujiona ana matiti mabaya, mfupi sana, mrefu sana ana matege, ana makengeza na kasoro nyingine zozote ambazo huhisi ni kosa kuwa nazo.
Nani amekuambia kuwa una kasoro? Mshukuru Mungu kwa kukuumba jinsi ulivyo, amini kuwa Mungu ana makusudi yake kukuumba kama ulivyo.
Kuna watu wengine wanaweza kukupenda kutokana na hizo kasoro unazoziona katika mwili wako!
Kujitoa kasoro na kutojiamini ni kosa kwa kuwa unakuwa unajiathiri kisaikolojia na kujiona hufai kupendwa mwisho wa yote unakuja kumparamia mtu yeyote kwa nia ya kujiondolea mkosi na akishakutumia anakuacha solemba unabaki na machungu moyoni na kujiongezea matatizo zaidi.
Naamini baada ya kujipenda wewe na kujiamini kuwa unavutia, utakuwa katika hali ya kawaida kisaikolojia na wakati mwingine anaweza akajitokeza akupendaye na kukuomba hifadhi ya moyo wake kwako.
Sababu ya kukaa muda mrefu bila mpenzi au kutamkiwa kuwa unapendwa isiwe chanzo cha kupata maumivu mapya ya moyo. Kuachwa kwako, kusiwe chanzo cha kuingia kwa mwingine ambaye anaweza kuwa mwiba zaidi.
Acha papara, tulia, pata wasaa wa kumchunguza huyo anayedai anakupenda kwa muda wa kutosha kwa kuwa inawezekana naye akawa ni mmoja kati ya wale wanaotaka kukufanya chombo cha starehe!
Akikuhitaji kuwa na wewe (huyo mwanaume)lazima umchunguze kwanza na usiruhusu aujue mwili wako kabla ya kuelewa nia yake hasa kwako ni ipi; starehe ya muda mfupi au anakuhitaji kimaisha.
Usifanye mambo kwa papara, unahitaji utulivu wa kutosha ili uweze kumpata yule ambaye ni muhimu kwa ajili yako.
 Ukijiamini na kuwa makini ni wazi kuwa utampata yule anayekupenda kwa dhati. Bila shaka tumeelewa.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...