31 May 2012


Biblia hamsini zilichomwa moto Zanzibar – Askofu Kaganga

VIONGOZI wa makanisa wa Zanzibar wametoa malalamiko yao ya vitendo vya uchomaji na uharibifu wa makanisa kisiwani humo na kutaja vitendo 23 huku wakiitaka Serikali kuingilia kati, Katibu wa umoja wa Wachungaji wa Zanzibar Jeremiah Kobero alisema kuwa licha ya makanisa matatu yaliyochomwa na kubomolewa katika vurugu za sasa, kuna matukio 23 ya uchomaji moto makanisa yametokea tangu mwaka 2001.

Aliyataja matukio hayo kuwa ni pamoja na uchomwaji moto wa makanisa ya The Church of God na Siloam yaliyofanyika mwaka 2011, makanisa mawili yaliyoko Masunguni yote mwaka huo huo, Kanisa la EAGT la Fuoni mwaka huo, kanisa la Pefa mwaka 2009, kanisa la Mwera mwaka 2012, kanisa la Redeemed lililiopo Dilikane mwaka 2001 yote ya mkoa wa Mjini Magharibi.

Alitaja pia makanisa yaliyochomwa katika mkoa wa Kaskazini kuwa kanisa la Tunguu, Unguja Ukuu, kanisa la CMF, Chukwani na Manyanya. Alitaja pia kuwepo kwa tabia hiyo kisiwani Pemba akisema kuwa imekuwa ni tabia kwa wakristo kusumbuliwa.

Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la TAG Kariakoo Zanzibar Dickson Kaganga aliwataka Viongozi wa serikali kuchukua tahadhari mapema kabla vurugu hazijatokea.

“Wakristo tumewafundisha kuvumilia…juzi walipovamia hapa walichoma moto biblia 50, ingekuwaje sisi tungechoma japo kitabu kimoja cha Kurani? Hayo makanisa yote yaliyochomwa, taarifa ziko polisi, lakini ukienda kutoa taarifa unaulizwa, una kibali? Yaani wanakutafutia tena kosa” alisema Askofu Kaganga.

Kaganga ambaye wakati wote alikuwa akibubujikwa na machozi aliwataka Wazanzibar kutambua umuhimu wa muungano kuwa ni pamoja na kuenezwa kwa dini. “Unapoona makanisa yanaenea hapa, ujue na kule bara misikiti inaenezwa na Wapemba ambao ni wajasiri wa biashara. Hiyo ndiyo faida ya muungano ndiyo faida ya kuoleana” alisema.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa askofu wa TAG kitaifa Askofu Magnus Mhiche alihoji kitendo cha wahuni kuvamia makanisa ilihali Serikali ikiwepo madarakani, “Mimi siamini kama ni Waislamu wamefanya haya, ila najiuliza, kama siyo wao basi ni wahuni. Hivi kweli wahuni wanatawala Zanzibar?” alihoji.

Naye Askofu wa kanisa kuu la Anglican Michael Hafidhi aliiomba Serikali kudhibiti mahubiri yanayotukana dini ya kikristo kwa njia ya kaseti akidai kuwa yanachochea vurugu.

“Zipo Kaseti zinazotukana ukristo, zinachochea vurugu, tunaomba serikali idhibiti. Hata ile kamati yetu ya ushirikiano wa dinio nayo imekufa inabidi ifufuliwe.

Kwa upande wake mwakilishi wa ofisi ya Mufti wa Zanzibar Thabit Jongo aliwataka Waislamu kuchukuliwana na Wakristo akisema kuwa hata Mtume (SAW) alifanya hivyo wakati akiitetea dini yake. “Hata Mtume wetu alipopata taabu alipokuwa Madina alikimbilia kwa Wakristo. Mpaka uislamu ulipoenea Makka yote. Hata alipotoka Medina na kwenda Mecca aliyempeleka hakuwa muislamu. Nashangaa leo ninaposikia eti Waislam wanachoma makanisa” alisema Jongo na kuongeza, “Hawa ni waislamu gani, mbona wamechoma hata bendera ya CCM, wamechoma bar na kunywa bia. Nini hasa malengo yao?

WAZIRI wa nchi katika Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mohamed Aboud amepiga marufuku mihadhara na maandamano yanayofanywa na vikundi vinavyopinga muungano akisema kuwa watawachukulia hatua kali za kisheria.

Waziri Aboud aliyasema jana hayo baada ya kutembelea kanisa la Assemblies Of God lililopo eneo la Karikoo mjini Zanzibar lililochomwa moto na kubomolewa kutokana na vurugu zilizozuka kufuatia kukamatwa kwa viongozi na wanachama wa kundi la Jumuiya za mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Uamsho). Katika ziara hiyo ambayo aliongozana na Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Said Mwema na Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa, Waziri Aboud alisema baadhi ya viongozi wa dini wanatoa maneno ya uchochezi yanayosabaisha vurugu.

“Baadhi ya viongozi wa dini wanatoa maneno ya uchochezi, yanachochea vurugu zote hizi…. Maneno ni sumu, ndiyo tumeiingiza nchi katika machafuko yote haya” alisema Waziri Aboud na kuongeza, “Sisi kama Serikali tumewaita wenye makundi hayo na kuzungumza. Tumewaambia, kama mtu hataki dini aje kwenye majukwaa ya siasa. Tumekosea kuwaachia watu waanzishe vyama na vimesajiliwa kisheria kwa lengo la kueneza dini, lakini sasa wanaleta uchochezi.

“Kuanzia sasa ni marufuku kufanya maandamano na mikusanyiko yoyote ya aina hiyo” alisisitiza Waziri Aboud. Naye IGP Said Mwema alisema kuwa jeshi hilo limeongeza ulizni katika maeneo maalum yenye usalama mdogo hasa makanisa.

“Tumejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa tunadhibiti maeneo maalum ili yasiendelee kuvamiwa. Tunafanya uchunguzi, ili kuhakikisha nani, kwa nini na wako wapi” alisema IGP Mwema. Alisema jeshi hilo kwa sasa lina kikosi maalum kwaajili ya kuongeza nguvu ya kudhibiti machafuko kisiwani humo na kwamba hadi jana jeshi hilo lilikuwa limekamata watu 46 na kati yao 43 wamefikishwa mahakamani huku wengine watattu wakifanyiwa uchuguzi.

Aidha IGP Mwema alikiri kwamba jeshi hilo limecghelewa kuzuia uhalifu huo na kwamba hatua iliyopo sasa ni kudhibiti usiendelee.

“Kuna mifumo mitatu ya ulinzi, kwanza ni kuzuia kabla mambo hayajatokea, kwa hapo sisi tumeshachelewa. Tuko hatua ya kudhibiti yasiendelee na baada ya hapo tutajenga amani iwe endelevu” alisema. Wakati huo huo Chama Cha Mapinduzi CCM kimesikitishwa na vurugu zilizotokea ambazo wanaamini kuwa zimeandaliwa na Jumuiya za Uamsho na kuitaka serikali kuchukua tahadhari kubwa katika suala hilo kwani kama hatua hizio hazijachukuliwa huenda likaleta maafa makubwa.

“Cham cha Mapinduzi kinaalani vitendo hivyo na kuzitaka serikali zote kudhibiti hali ya amani na utulivu tulioizowea na kuwachukulia hatua kali wote waliosababisha vurugu hizi” alisema taarifa yake kwa vyombo vya habari. Kwa upande wake chama cha Chadema kimelaani vurugu hizo zilizofanywa kwa makusudi na vijana ambao wanaonekana wameshapata mafunzo maalumu kwa kusaidiwa na chama kimoja cha kisiasa kinachounda serikali ya umoja wa kitaifa.

“Chadema tunavitaka vyama vya siasa kuandaa makundi ya vijana ambayo mwisho wake wanakosa kuwapatia kazi na hatima yake kuwa vikundi vya kihalifu nchini” ilisema taaifa hiyo iliyotiwa saini na Hamad Yussuf Naibu Katibu Mkuu.
Chama Cha Wananchi CUF kimelaani vurugu hizo na kusema zimesababishwa na chuki binfasi, ukosefu wa hekima, matumizi ya nguvu za dola na uchochezi wa makusudi kwa wale wasiopendeleaq maridhiano ya kisiasa ya Zanzibar.

“Vitendo vya watu wachache na kuharibu mali za watu ni uvunjifu wa sheria na kinyume na utamaduni wa kizanzibari, uchunguzi wa kina ufanyike na waliohusika wachukuliwe hatua bila ya uonevu wala upendele” imesema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Salim Bimani

sosi: zanzibaryetu            

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...