04 June 2012

Kikwete Asema Muungano hauvunjwi kwa kuchoma makanisa

Rais Jakaya Mrisho Kikwete



RAIS Jakaya Kikwete amesema vitendo vilivyofanywa na wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam Zanzibar (JUMUKI) visiwani humo havikubaliki wala havivumiliki na kusisitiza kwamba, kuwepo au kutokuwepo kwa muungano hakuwezi kudaiwa kwa kuchoma moto makanisa.

Katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi aliyotumwa jana kwa vyombo vya habari, Rais Kikwete alisema; “Haipendezi Serikali ikichukua  hatua kali dhidi ya raia wake, lakini  kama itashindikana haitasita kufanya hivyo.

“Nawasihi viongozi na wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho kurejea kwenye madhumuni ya msingi ya jumuiya yao, wajiepushe na ajenda za kisiasa na kupandikiza chuki zitakazosababisha mifarakano baina ya wananchi wa pande zetu mbili za Muungano na baina ya Wakristo na Waislamu.”Mbali na kuzungumzia vurugu hizo za Zanzibar, Rais Kikwete ameeleza  kilichojiri katika mkutano wa nchi tajiri duniani (G8) na ule wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), huku akiunga mkono kauli ya Rais wa Zanzibar, Dk  Ali Mohamed Shein ya  kulaani vurugu visiwani humo.

Alisema kuwa ghasia hizo zimechochewa na viongozi wa Jumuiya hiyo ambayo ilianzishwa kwa madhumuni ya kidini, lakini hivi sasa imeacha madhumuni hayo na kubeba ajenda za siasa.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja siku moja baada ya Kiongozi Mkuu wa Jumuiya hiyo ambaye pia anadaiwa kuwa mfadhili wa kundi hilo, Sheikh Azzan Khalid Hamdan kukamatwa na polisi visiwani humo muda mfupi baada ya kuwasili akitokea Oman.

Wakati Sheikh huyo akiwa safarini Oman, Zanzibar yalifanyika  maandamano makubwa yaliyoambatana na kuchomwa moto kwa makanisa pamoja na vitu mbalimbali kuharibiwa.
Katika hotuba yake Rais Kikwete alisema; “Siku za nyuma walikuwa wakitumia muda mwingi kuilaumu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa lawama hizo sasa hazisikiki.

“Tulipoanzisha mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mihadhara yao imeelekezwa kupinga Muungano na kuwakashifu viongozi waasisi wa Muungano na hata waliopo sasa.” Alisema watu hao wamekuwa wakipandikiza chuki kwa ndugu zao kutoka Tanzania bara pamoja na wafuasi wa dini ya Kikristo.

Alisema vitendo vya kuchoma moto makanisa na uhalifu haviwezi kufanywa kwa hoja ya kupinga muungano na kwamba Ukristo haukuingizwa Zanzibar na muungano bali ulikuwepo karne kadhaa kabla ya muungano na wala haukutokea Tanzania Bara.
“Kama alivyoeleza Rais Shein, ukweli ni kwamba, dini ya Kikristo kama ilivyo ya Kiislamu imeenezwa Bara kutokea Zanzibar.  Kanisa kuu la Anglikana Zanzibar lilijengwa kuanzia mwaka 1873 na lile la Katoliki kuanzia 1893 ni miongoni mwa Makanisa makongwe kuliko mengi kama siyo yote kwa upande wa Zanzibar na Bara” alisema Rais Kikwete.

Alisema kuwa matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mtu kuwa huru  wa kuchagua au kubadilisha dini, kwamba yanayofanywa na jumuiya hiyo kwa kisingizio cha Muungano ni jambo lisiloeleweka kabisa na wala halina mantiki na kusisitiza; “Labda kama wana ajenda nyingine”.

Aliongeza: “Jambo la kushangaza ni kutokea vurugu na ghasia wakati ambapo Serikali imetoa fursa  kwa watu kutoa maoni yao kwenye mjadala wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Tume ya kukusanya maoni imeshaundwa na inajiandaa kwa kazi hiyo, utaratibu mzuri umeshawekwa sasa vurugu za nini,” alihoji rais Kikwete.
Alisema kuwa hakuna sababu ya msingi kwa watu kusababisha uvunjifu wa amani kwa kuwa hali hiyo inaharibu sifa na sura ya Wazanzibari na Watanzania.

Alisema kuwa Watanzania ni ndugu na wamekuwa wakiishi pamoja kwa furaha licha ya tofauti zao  za rangi, makabila, dini na maeneo watokako.Katika hotuba yake Rais Kikwete aliwapa pole wananchi walioathirika na vurugu hizo na kwamba serikali itahakikisha kuwa wananchi wanakuwa salama pamoja na mali zao.
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...