08 March 2012

Vita Vya Kiroho 2


Tunaendelea


2 Wakorintho 2:11 “Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake”.


Mwl Patrick Sanga
Shetani anajua kabisa kwamba hawezi kukushinda kama unaishi kwa kutii na kulifuata neno la Mungu. Maana anajua imeandikwa (Warumi 2:13) si kila asikiaye sheria ndiyo mwenye kuhesabiwa haki bali ni yule aitendaye sheria … na pia anajua imeandikwa Basi mtiini Mungu. Mpingeni shetani, naye atawakimbia.  

Sasa fikra zake kwa maana ya vita vya kiroho ni kuhakikisha ana kutengenezea mazingira ya wewe kuasi au kutotii neno la Mungu. Mungu hana namna ya kukusaidia kama hauko tayari kutii neno lake.

2 Wakorinto 10:3-6 “ Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome, tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu, na tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo’.

Yohana 10:10 ‘Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu…
Vita vya kiroho vinaanzia kwenye wazo. Na mwenye kuleta hilo wazo ni shetani. Yeye huja kwa wazo, akitambua kwamba ndani yako kuna wazo jingine bora la Mungu, na kwa hiyo mkakati wake ni kuondoa hilo wazo bora kwa wazo la uharibifu.

Katika sehemu hii ya pili mpenzi msomaji ninataka kukuonyesha kwamba Shetani katika kuvipiga vita vya kiroho anatumia hila. Hila ni mkakati mkubwa sana na wa mwisho ambao siku zote Shetani huutumia katika mapambano yake dhidi ya watoto wa Mungu. Mkakati huu ndio ambao watu wengi wameshindwa kuujua na hivyo kujitkuta wakianguka katika dhambi za namna mbalimbali na kuharibu kusudi la Mungu kwako.


Unajua ni kwa nini?  Ni kwa sababu Shetani naye hujigeuza kama malaika wa nuru na kufanya kutoka kwenye kona ya malaika wa nuru kumbe yeye ni malaika wa giza. Si hivyo tu bali Shetani huja kwa njia ya neno kana kwamba ni Bwana na kwa kuwa si wengi wenye elimu ya ufalme wa mbinguni hupotea. Zaidi Shetani huja kama mwana kondoo lakini ndani yake ni umbwa mwitu. Nasikitika kusema kwa njia hizi amewanasa wengi sana.

 Kumbuka Shetani anapokuja haijalishi anakuja kwa sura gani iwe kondoo/malaika nk. lengo lake ni kuleta uharibifu mkubwa kabisa. Shetani kwa upande mwingine ni mzoefu wa vita, hajaanza leo, amepigana vita nyingi sana na za kila aina nyingine ameshinda na nyingine ameshindwa (kama wewe ni msomaji wa Biblia utaniunga mkono).Vita anayopigana Shetani kwa mfumo wa hila mara nyingi sio vita ambayo matokeo yake ni ya siku hiyo hiyo.  

Anaweza akaandaa leo hila kama mkakati wa uharibifu ambao matokeo yake utayaona baada ya mwezi mmoja, mitano au miaka kadhaa mbele. Fahamu kwamba  mkakati  wa hila mara nying unalenga ‘future’ yako. Mfano Shetani anapokupa mume/mke nje ya kusudi la Mungu. Wapambe watapiga vigele vigele na kusema hakika Bwana amefanya na mnatoa na sadaka ya shukrani. Baada ya miezi kadhaa yanazaliwa mambo kwa hao wanandoa ambayo kila mtu anakataa kuyaelezea.

Wakati mwingine anaweza akaja mgeni kanisani kwenu akajitambulisha vizuri, nanyi kwa upendo mkamkaribisha na kwenye kwaya/Umoja wa vijana/Wamama/Wababa nk.  Na kwa sababu ya jitihada zake kwenye Mahudhurio/maombi/mazoezi  mkampa na uongozi kwenye umoja wenu.  

Baada ya miaka kadhaa sasa mnajuta, msijue kwamba wengine ni watumishi wa adui ambao wanapandwa kwenye kila eneo tayari kwa kazi yake. Kanisa sikia, Shetani amemwaga watu wengi makanisani ambao sio rahisi kuwajua maana wamevaa vazi la kondoo na kujivika taa ya malaika wa nuru. Bila kuwa macho kanisa litakwisha.

Mara nyingi, kama mtumishi anaandaa ujumbe kwa ajili ya huduma ya mkutano/semina au hata ibada ya kawaida tuseme ya jumapili.  Shetani akijua kwamba huyo mtumishi ni mmoja wa wale wanaokaa barazani pa Bwana ili awasikizishe kitu cha kusema na watu wake, basi Shetani kuna vitu vingi sana atafanya hapa kati kati ili kuzuia ule ujumbe usiwafikie walengwa. Mfano anaweza akaleta ugomvi toka ndani ya familia, ndoa, kanisa nk. 

Anaweza hata kuleta msiba unaomhusu huyo ndugu, anaweza akatengeneza hata mazingira ya safari/mwaliko wa kwenda nje huyo mtumishi. Sasa yeye bila kujua akidhani ni Bwana anampanga mtu mwingine kuhudumu badala yake au kuhairisha kama ni mkutano au semina. Shetani atapambana kuhakikisha kile ambacho Mungu alitaka kusema na kufanya kupitia huyo ndugu hakifanikiwi (Asomaye na afahamu).


Kwa mfumo huu wa hila Shetani hapigi kila mahali, nimekuambia kwamba huu ndio makakati mkubwa sana ambao yeye mwenyewe anauamini na kuutumia. Shetani anapotaka kupiga yuko makini kupiga eneo ambalo anajua akipiga anaharibu wengi.  Mfano, Shetani anapowafusha watumishi wa Mungu sasa kwa njia ya fedha na zinaa na kuwafanya washindwe kuisema kweli yote ya injili, kuwafanya wasilionye/kukemea dhambi na uovu ndani ya kanisa. Shetani anawafanya watumishi wengi kuwatumainisha watu kwamba Yesu ni wa rehema tu atawabariki na siku wakifa wataenda mbinguni hata kama maisha yao yamejaa dhambi. 

Nasikitika kusema kuna baadhi ya watumishi wametoka kwenye Injili ya kweli na sasa wanahubiri na kufundisha mawazo ya moiyo yao na kuwaaaminisha wafuasi wao kwamba Mungu ndiye anayesema kupitia wao (Yeremia 23:13-22). Kumbuka Shetani anapiga Mchungaji ili kutawanya kondoo/ anapiga mlinzi ili kuwaacha raia katika hali ya kuvamiwa ki u rahisi.
Itaendelea..

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...