Pages

18 May 2013


MIRIAM LUKINDO: Mwimbaji wa nyimbo za Injili, mpambaji



MIRIAM Lukindo ni miongoni mwa wanamuziki mahiri wa nyimbo za injili nchini ambaye amekuwa akijihusisha pia na masuala ya upambaji katika matukio mbalimbali hata maofisini.Mwanadada huyo alikulia katika Jiji la Mbeya, alikokuwa akiishi yeye na mama yake pamoja na bibi yake. 
Miriam alisoma Shule ya Msingi Kilimo Uyole na kufanikiwa kuendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Sekondari Majengo iliyoko katikati ya mji wa Moshi.
Mama yake alipata ujauzito wa Miriam akiwa kidato cha pili, kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 16.

Katika kipindi chote hicho tangu akiwa mdogo, Miriam alikuwa akipenda sana kuimba na akipenda kusikiliza nyimbo za Rebeka Malope, nguli wa nyimbo za injili wa Afrika Kusini.
Miriam hakuwahi kumfahamu baba yake japokuwa aliambiwa kuwa yupo. Jambo hilo lilimuumiza na ilifikia hatua akaona ni hali ya kawaida hivyo chochote kuhusu yeye bibi yake na mama yake ndio walikuwa kila kitu kwake.

Desemba, 1995 kwa mara ya kwanza Miriam alipata fursa ya kuonana ana kwa ana na baba yake mzazi mzee Lukindo.

Miriam anasema pamoja na maongezi yote anakumbuka alimwambia babaye neno moja la msingi kwamba: “Nimefurahi kukujua. ”
Baada ya kuhitimu masomo ya sekondari, Miriam alipata nafasi ya kuendelea na masomo ya chuo Nairobi, Kenya. Kwa mujibu wa Miriam, akiwa nchini humo ndipo hasa kipaji chake cha uimbaji kiliweza kuchanua vizuri.

Akiwa nchini Kenya alikuwa akisali katika Kanisa la Maximum Miracle Centre lililo chini ya Mchungaji na muimbaji mahiri nchini humo aitwaye Pastor Pius Muiru.
Anasema chini ya Pastor Muiru, alikuwa kiongozi wa sifa na kuabudu kanisani hapo. Kanisa hilo ndilo mzizi wa kundi maarufu la muziki wa injili nchini humo liitwalo Maximum Melody.

Katika kipindi hicho Miriam anasema alipitia masaibu mengi ya kumkatisha tamaa kimaisha lakini Kristo alikuwa akimtetea na hatimaye alifanikiwa kurekodi albamu yake ya kwanza aliyoiita ‘Amen Amen’ mwaka 2000.

Baada ya kurekodi albamu hiyo nchini Kenya, Miriam aliamua kurudi Tanzania, kwa kuwa baba yake na mama yake hawakuwa pamoja lakini bibi yake akiwa Mbeya, ilimuwia vigumu namna ya kuweza kuishi katika Jiji la Dar es Salaam.

Kwa bahati rafiki yake mmoja alikubali kuishi naye katika kipindi hicho, Miriam aliamua kufanya huduma kwa nguvu na albamu yake ilikubaliwa vema na watu mbalimbali, hivyo kwa sehemu ikawa faraja kwa Miriam.
Haya ni baadhi ya maswali ambayo nilimuuliza mwanamuziki huyu naye bila shaka akatanabaisha majibu.

Mwandishi: Changamoto gani unakutana nazo?

Miriam: Unajua wakati mwingine unapotakiwa kuishi kwa kukabiliana na majukumu mengi, unatumika na bado unajali familia ni vitu viwili vigumu sana, kwa sababu sisi wanawake unakuta wakati mwingine unakuwa mjamzito, huwezi kusafiri na hapohapo unatakiwa ufanye huduma hapohapo karibu.Ama wakati mwingine umejifungua mtoto ni mdogo, huwezi kuanza kuzurura naye mikoani, kwa hiyo inabidi utulie kwanza. Sasa muda ambao unatulia ni changamoto kubwa sana kwa sababu, ule muda unaotulia, vitu vingi vinapita, kwangu hii huwa inakuwa changamoto kidogo.

Mwandishi: Ulikuwa ukisafiri maeneo mbalimbali na kampeni yako ya kusaidia watoto wasiojiweza na hasa wenye ulemavu wa akili, vipi bado unaendelea na huduma yako?

Miriam: Changamoto niliyonayo sasahivi kwa kweli nakosa pesa kwa ajili ya kuwaendea kijijini hawa watu, lakini bado ile kampeni yangu kimya kimya naendelea nayo pale ninapokuwa na uwezo nafanya.


Mwandishi: Miriam umeshauza kopi ngapi mpaka sasa za nyimbo zako?

Miriam: Kabla sijaja Tanzania nilikuwa nimeshauza kopi 6,000 Nairobi, na nilipokuja sikuwa na yale mahesabu kamili kwa sababu unakuta wakati umempa mtu yeye ndo anaifanyia kazi, kwa hiyo yeye ndo anajua kwamba ameuza ngapi.

Mwandishi: Umekuwa kimya muda mrefu kidogo, kulikoni?

Miriam: Aaaah! Unajua nilikuwa nalea, sasa nina mtoto si mkubwa sana, kwa hiyo nikawa nafanya mambo chinichini ambavyo si sana kwa sababu ya kumlea mtoto, kwa hiyo mashabiki wangu wanipe muda kidogo tu halafu wataona mambo yatakuwa mazuri kabisa.

Mwandishi: Miriam umeolewa nafahamu hilo, lakini una watoto wangapi na vipi kuhusu tungo zako, nani anakutungia?

Miriam: Kwa sasa nina watoto wawili Mungu amenijalia watoto wa kike Romy wa kwanza na Romelle, mume wangu ni Chriss Mauki, ambaye ni ‘director’ wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anafundisha saikolojia. Lakini mimi situngiwi ila huwa namshangaa Mungu katika tungo zangu.Kwa mfano kuna nyimbo nyingine ambayo haichukui muda kutunga, unaweza ukawa umenijia nikauandika, labda baada ya siku mbili tatu tena nikauandika vizuri ukawa umeshaisha hiyo ni neema tu namshukuru Mungu kwa ajili ya hilo kwa kweli.

Mwandishi: Vipi, bado unaendelea na uimbaji wa ‘live’, na vipi kuhusu kufanya shoo za ‘live?’

Miriam: Kwa sasa nilikuwa najipanga kwa ajili ya hizo ‘concert’ za ‘live’, lakini kwa wale ambao huwa wanakuja FOF (Friends on Friday) kila mwanzo wa mwezi basi wataniona kwa sababu huwa tunapiga.

Miriam: Aaah! Hiyo ni challenge kubwa sana bwana, aaahm, kumiliki bendi ni kitu kinachotakiwa kujipanga sana bwana, si kitu kidogo kwa kweli. Lakini kupiga ‘live’ huwa napiga ‘live’, na wako wapigaji ambao huwa napiga nao ‘live’, lakini bado siwezi kuwamiliki, nawatumia pale wakati ninapotaka kuwatumia labda kwenye mazoezi, au ninapoenda kupiga mahali, lakini kuwamiliki kwamba ni wa kwangu au kuwa na bendi yangu, bado haijafikia hapo. Na wanatakiwa kuelewa, hata wasanii wa nje si kwamba wanamiliki bendi, ndio maana utaona wale waimbaji walioimba na Solly Malangu sijui wameimba na Joyous na wengine na Rebecca Malope, yaani ni waimbaji ambao wapo wanashirikiana. Aaam, yaani kumiliki bendi si kitu kidogo, ni kitu kikubwa sana, kwa hapo sijafikia, Mungu atakapotuwezesha kwa hapo basi hilo tutalifanya, lakini kwa sasa bado.

Mwandishi: Umemshirikisha muimbaji kutoka Zambia, Ephraim Sekeleti, ulimpataje na ilikuwaje mpaka ukashirikiana naye?

Miriam: Ephraim nilikuwa natamani kufanya nae kazi tangu nilipomsikia katika albamu yake ya kwanza, lakini sikujua nitampataje.

Nakumbuka nilikuwa tu namwambia mume wangu: "Huyu kaka natamani nifanye naye kazi. Ikatokea kwamba huo wimbo mimi niliupata, nikatengeneza muziki, nikauimba wote nikamaliza, lakini kila ninaporudi studio naona huu wimbo hautakiwi kutoka hivi, kila nikirudi naimba tena naambiwa hapana, ‘director’ wangu ananiambia bado hujafanya kinachotakiwa. Nikamuuliza sana Mungu huu wimbo naufanyaje?
Muimbaji Sekeleti ameuchukua wimbo huo na kwenda kuufanyia ‘mixing’ na Miriam anaeleza kuwa albamu yake itakuwa bomba na bora ambapo inatarajiwa kutoka Agosti mwaka huu.

No comments:

Post a Comment