VIONGOZI wa makanisa wa Zanzibar wametoa
malalamiko yao ya vitendo vya uchomaji na uharibifu wa makanisa
kisiwani humo na kutaja vitendo 23 huku wakiitaka Serikali kuingilia
kati, Katibu wa umoja wa Wachungaji wa Zanzibar Jeremiah Kobero alisema
kuwa licha ya makanisa matatu yaliyochomwa na kubomolewa katika vurugu
za sasa, kuna matukio 23 ya uchomaji moto makanisa yametokea tangu mwaka
2001.
Aliyataja matukio hayo kuwa ni pamoja na
uchomwaji moto wa makanisa ya The Church of God na Siloam yaliyofanyika
mwaka 2011, makanisa mawili yaliyoko Masunguni yote mwaka huo huo,
Kanisa la EAGT la Fuoni mwaka huo, kanisa la Pefa mwaka 2009, kanisa la
Mwera mwaka 2012, kanisa la Redeemed lililiopo Dilikane mwaka 2001 yote
ya mkoa wa Mjini Magharibi.
Alitaja pia makanisa yaliyochomwa katika mkoa wa Kaskazini kuwa
kanisa la Tunguu, Unguja Ukuu, kanisa la CMF, Chukwani na
Manyanya. Alitaja pia kuwepo kwa tabia hiyo kisiwani Pemba akisema kuwa
imekuwa ni tabia kwa wakristo kusumbuliwa.
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la TAG
Kariakoo Zanzibar Dickson Kaganga aliwataka Viongozi wa serikali
kuchukua tahadhari mapema kabla vurugu hazijatokea.
“Wakristo tumewafundisha kuvumilia…juzi walipovamia hapa walichoma
moto biblia 50, ingekuwaje sisi tungechoma japo kitabu kimoja cha
Kurani? Hayo makanisa yote yaliyochomwa, taarifa ziko polisi, lakini
ukienda kutoa taarifa unaulizwa, una kibali? Yaani wanakutafutia tena
kosa” alisema Askofu Kaganga.
Kaganga ambaye wakati wote alikuwa
akibubujikwa na machozi aliwataka Wazanzibar kutambua umuhimu wa
muungano kuwa ni pamoja na kuenezwa kwa dini. “Unapoona makanisa
yanaenea hapa, ujue na kule bara misikiti inaenezwa na Wapemba ambao ni
wajasiri wa biashara. Hiyo ndiyo faida ya muungano ndiyo faida ya
kuoleana” alisema.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa askofu wa TAG kitaifa Askofu Magnus
Mhiche alihoji kitendo cha wahuni kuvamia makanisa ilihali Serikali
ikiwepo madarakani, “Mimi siamini kama ni Waislamu wamefanya haya, ila
najiuliza, kama siyo wao basi ni wahuni. Hivi kweli wahuni wanatawala
Zanzibar?” alihoji.
Naye Askofu wa kanisa kuu la Anglican Michael Hafidhi aliiomba
Serikali kudhibiti mahubiri yanayotukana dini ya kikristo kwa njia ya
kaseti akidai kuwa yanachochea vurugu.
“Zipo Kaseti zinazotukana ukristo,
zinachochea vurugu, tunaomba serikali idhibiti. Hata ile kamati yetu ya
ushirikiano wa dinio nayo imekufa inabidi ifufuliwe.
Kwa upande wake mwakilishi wa ofisi ya Mufti wa Zanzibar Thabit
Jongo aliwataka Waislamu kuchukuliwana na Wakristo akisema kuwa hata
Mtume (SAW) alifanya hivyo wakati akiitetea dini yake. “Hata Mtume wetu
alipopata taabu alipokuwa Madina alikimbilia kwa Wakristo. Mpaka uislamu
ulipoenea Makka yote. Hata alipotoka Medina na kwenda Mecca
aliyempeleka hakuwa muislamu. Nashangaa leo ninaposikia eti Waislam
wanachoma makanisa” alisema Jongo na kuongeza, “Hawa ni waislamu gani,
mbona wamechoma hata bendera ya CCM, wamechoma bar na kunywa bia. Nini
hasa malengo yao?
WAZIRI wa nchi katika Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar Mohamed Aboud amepiga marufuku mihadhara na
maandamano yanayofanywa na vikundi vinavyopinga muungano akisema kuwa
watawachukulia hatua kali za kisheria.
Waziri Aboud aliyasema jana hayo baada
ya kutembelea kanisa la Assemblies Of God lililopo eneo la Karikoo mjini
Zanzibar lililochomwa moto na kubomolewa kutokana na vurugu zilizozuka
kufuatia kukamatwa kwa viongozi na wanachama wa kundi la Jumuiya za
mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Uamsho). Katika ziara hiyo ambayo
aliongozana na Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Said Mwema na Kamishna wa
Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa, Waziri Aboud alisema baadhi ya viongozi
wa dini wanatoa maneno ya uchochezi yanayosabaisha vurugu.
“Baadhi ya viongozi wa dini wanatoa maneno ya uchochezi, yanachochea
vurugu zote hizi…. Maneno ni sumu, ndiyo tumeiingiza nchi katika
machafuko yote haya” alisema Waziri Aboud na kuongeza, “Sisi kama
Serikali tumewaita wenye makundi hayo na kuzungumza. Tumewaambia, kama
mtu hataki dini aje kwenye majukwaa ya siasa. Tumekosea kuwaachia watu
waanzishe vyama na vimesajiliwa kisheria kwa lengo la kueneza dini,
lakini sasa wanaleta uchochezi.
“Kuanzia sasa ni marufuku kufanya
maandamano na mikusanyiko yoyote ya aina hiyo” alisisitiza Waziri
Aboud. Naye IGP Said Mwema alisema kuwa jeshi hilo limeongeza ulizni
katika maeneo maalum yenye usalama mdogo hasa makanisa.
“Tumejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa tunadhibiti maeneo maalum
ili yasiendelee kuvamiwa. Tunafanya uchunguzi, ili kuhakikisha nani, kwa
nini na wako wapi” alisema IGP Mwema. Alisema jeshi hilo kwa sasa lina
kikosi maalum kwaajili ya kuongeza nguvu ya kudhibiti machafuko kisiwani
humo na kwamba hadi jana jeshi hilo lilikuwa limekamata watu 46 na kati
yao 43 wamefikishwa mahakamani huku wengine watattu wakifanyiwa
uchuguzi.
Aidha IGP Mwema alikiri kwamba jeshi hilo limecghelewa kuzuia uhalifu huo na kwamba hatua iliyopo sasa ni kudhibiti usiendelee.
“Kuna mifumo mitatu ya ulinzi, kwanza ni kuzuia kabla mambo
hayajatokea, kwa hapo sisi tumeshachelewa. Tuko hatua ya kudhibiti
yasiendelee na baada ya hapo tutajenga amani iwe endelevu”
alisema. Wakati huo huo Chama Cha Mapinduzi CCM kimesikitishwa na vurugu
zilizotokea ambazo wanaamini kuwa zimeandaliwa na Jumuiya za Uamsho na
kuitaka serikali kuchukua tahadhari kubwa katika suala hilo kwani kama
hatua hizio hazijachukuliwa huenda likaleta maafa makubwa.
“Cham cha Mapinduzi kinaalani vitendo
hivyo na kuzitaka serikali zote kudhibiti hali ya amani na utulivu
tulioizowea na kuwachukulia hatua kali wote waliosababisha vurugu hizi”
alisema taarifa yake kwa vyombo vya habari. Kwa upande wake chama cha
Chadema kimelaani vurugu hizo zilizofanywa kwa makusudi na vijana ambao
wanaonekana wameshapata mafunzo maalumu kwa kusaidiwa na chama kimoja
cha kisiasa kinachounda serikali ya umoja wa kitaifa.
“Chadema tunavitaka vyama vya siasa kuandaa makundi ya vijana ambayo
mwisho wake wanakosa kuwapatia kazi na hatima yake kuwa vikundi vya
kihalifu nchini” ilisema taaifa hiyo iliyotiwa saini na Hamad Yussuf
Naibu Katibu Mkuu.
Chama Cha Wananchi CUF kimelaani vurugu hizo na kusema zimesababishwa na
chuki binfasi, ukosefu wa hekima, matumizi ya nguvu za dola na
uchochezi wa makusudi kwa wale wasiopendeleaq maridhiano ya kisiasa ya
Zanzibar.
“Vitendo vya watu wachache na kuharibu
mali za watu ni uvunjifu wa sheria na kinyume na utamaduni wa
kizanzibari, uchunguzi wa kina ufanyike na waliohusika wachukuliwe hatua
bila ya uonevu wala upendele” imesema taarifa hiyo iliyotiwa saini na
Salim Bimani