Pages

20 March 2012

ULIMWENGU WA ROHO

Ijue Na Kuitumia Nafasi Yako Ya Ulinzi Katika Ulimwengu Wa Roho



Nakusalimu kwa jina la Yesu!,Biblia katika Ezekieli 33:7 inasema ‘Basi, wewe, mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli, basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu’.

Ukisoma habari hii kuanzia ule mstari wa kwanza hadi ule wa tisa, utaona namna Mungu alivyosema na Ezekieli kuhusu wajibu wa ulinzi aliokuwa amepewa kwa watu wa Taifa lake. 

Jukumu lake kama Mlinzi ilikuwa ni kutoa taarifa kwa wale anaowalinda.  Kila alipoona hatari alipaswa kutoa taarifa kwa wale anaowalinda. Kama mtu angekufa wakati mlinzi alitoa taarifa, damu yake, ilikuwa juu ya mtu huyo. Lakini kama akifa kwa kuwa mlinzi hukutoa taarifa basi damu yake ilidaiwa juu ya mlinzi husika. Naam jambo la msingi kujua ni kwamba kumbe mwanadamu amepewa kuwa mlinzi wa jambo fulani hapa dunaiani.

Isaya 62: 6-7 ‘Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Eee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya; wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani’.

Naam maandiko haya yanazidi kudhihirisha na kufafanua kuhusu nafsi ya ulinzi kwa mwanadamu. Hapa Mungu alikuwa anasema na mji wa Yerusalemu kwamba ameweka walinzi juu ya kuta zake, na kazi yao ni kumkumbusha Bwana afanye kile alichoahidi kufanya juu ya mji huo kwa kutokunyamaza usiku wala mchana. Hii ina maana mfumo wa ulinzi wa Walinzi hawa wa kuta za Yerusalemu ulikuwa kwa njia ya kinywa kama ilivyokuwa kwa Ezeikeli pia. Kwa vinywa vyao walionya, waliomba, walifundisha nk. Naam Walinzi hawa walijua wajibu wao ni  nini katika nafasi zao za maeneo yao ya ulinzi.

Ezekieli anatumbia kwa habari ya ‘mlinzi wa nyumba ya Israeli’ na Isaya anatuambia kwa habari ya ‘Walinzi wa kuta za Yerusalemu’. Tofauti hizi za ulinzi zinatujulisha kwa habari ya nafasi mbalimbali alizonazo mwanadamu katika ulimwengu wa roho.

Nyumba ya Israeli’ na ‘Kuta za Yerusalemu’ ni maeneo ya ulinzi, au maeneo yanayohitaji kulindwa na hivyo yanahitaji walinzi. Hata sasa yapo maeneo mbalimbali ambayo ni nyumba ya Israeli na kuta za Yerusalemu kwa jinsi ya rohoni, ambayo yanahitaji ulinzi wa kipekee ili makusudi ya Mungu yaweze kufanikiwa. Fahamu kwamba ‘kufanikiwa kwa kusudi la Mungu duniani kunategemea utiifu wa ‘walinzi’ wake duniani kwenye nafasi ambazo amewapa katika ulimwengu wa roho’. Huu ni  mwanzo wa somo hili pana, endelea kufuatilia  mfululizo wa somo hili ili upate kujifunza kwa namna gani ‘mwanadamu umepewa kuwa mlinzi’  kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yako, watu wako, mji wako na Taifa lako nk.

Mungu akubariki, tutaendelea na shemu ya pili…

No comments:

Post a Comment